Monday, September 15, 2014

WATAPIGANA NA WEWE LAKINI HAWATAKUSHINDA

WATAPIGANA NA WEWE LAKINI HAWATAKUSHINDA

na   mzawa wa injili .....


“Nahisi siwezi kuendelea mbele kabisa. Napigwa vita kila kona. Naona tu nipumzike, sioni tumaini”. Ni maneno ya mtu aliye kata tamaa baada ya kukumbana na vita katika maisha yake. Kuna watu wengi waliookoka ambao walikuwa na malengo lakini hawakuweza kuyafikia baada tu ya vita kuwa  kubwa kwao na kuwaelemea. Swali la muhimu la kujiuliza hapa ni Je, ni kweli kuwa Mungu ameshindwa kumpigania huyu mtu kiasi cha yeye kukata tamaa namna hii? Jibu pekee linalo lingana na kweli ya neno la Mungu ni “HAPANA”, kwa nini? Soma na zingatia kwa makini mambo yafuatayo;

1. Mungu akiwa upande wetu hakuna aliye juu yetu (Rum 8:31). Hii inamaanisha kuwa kama sisi tumeshika haki (Isa 56:1) mwamuzi pekee katika maisha yetu ni Mungu na si mwanadamu. Sambamba na hilo tunatakiwa kuelewa kuwa hatuwezi kumwacha mwanadamu atuamulie sisi kuwa wenye haki au siyo. Mungu pekee ndiye mwenye kutuhesabia haki (Rum 8:33-34)

2. Mungu mwenyewe ameahidi kuwa kwetu sisi ushindi ni wa lazima, japokuwa watashindana na sisi hawawezi kushinda (Yer 1:19)

3. Ni lazima ujue kuwa vita kwako ni kawaida na siyo kama unaonewa na Mungu. Wakristo wengi wanapokuwa katika vita wanasahau kuwa hilo ni jambo la kawaida ili kuimarisha imani na utumishi wao kwa Mungu wao (Yak 1:12). Fahamu pia kuwa majaribu yanakufanya ukubaliwe na Mungu, ila kuyashinda ni lazima (Yak 5:8). 

 

Ili kujihakikishia ushindi;

Hakikisha una silaha zote (Ef 6:13-17). Hata katika vita vya kawaida kimwili, huwezi kwenda vitani ukitegemea kushinda ukiwa hauna silaha za kutosha au ukiwa hauna silaha kabisa. Katika dhana hiyo hiyo rohoni ni lazima uwe na silaha pia ili uweze kushinda.

Vita si vyako bali ni vya Mungu. Ni lazima ujue kuwa huwezi kupigana vita mwenyewe ukashinda kwa maana katika hali ya kawaida maadui wanaweza kuwa wengi na uwezo mkubwa kuliko wewe, hivyo Mungu tu ndiye anaweza kuwashughulikia. Hivi ndivyo Mungu alivyowaambia wana wa Israel (Kumb 20:1, 4)

Daima pigana vita vya kiroho si vya kimwili (Ef 6:12). Ni vizuri na ni lazima ujue pia  kuwa kila vita utakayo pigana nayo chanzo chake ni katika ulimwengu wa roho. Twaweza kuona matokeo mengi katika ulimwengu wa damu na nyama lakini tu haya yote yametokea katika ulimwengu wa roho. Usikubali hata siku moja kupigana vita vya kimwili katika safari hii tuliyo nayo.

Siku zote epuka kuwa mtu wa kulalamika na kunun’gunika unapokuwa vitani. Mungu hapendi watu wanao lalamika mara wanapokuwa katika vita (Hes 14:1…). Kulalamika kutakupotezea mwelekeo na hatimaye utashindwa vitani. Ni muhimu kumsifu Mungu hata katika magumu.

Muhimu sana….

Vita huwa ni kushambulia na kushambuliwa. Ukishambuliwa lazima ujue jinsi ya kujikinga usidhurike. Lakini pia lazima ushambulie, usiwe mtu wa kushambuliwa tu… utashindwa.VAA SILAHA” (Ef 6:11).

Mzawa wa injili, 0759210407,, mzawa wa injili livegospel. blogspot.com,, medardmaxwell@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment